UTOVU WA USALAMA WASALIA KIZUNGUMKUTI CHESOGON, WAKAZI WAKIPAZA VILIO.
Wakazi wa Cheptulel eneo la Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet wamelalamikia kukithiri utovu wa usalama ambao unasababishwa na uvamizi wa mara kwa mara wa wezi wa mifugo.
Wakizungumza na wanahabari wakazi hao walisema kwamba maboma mengi yamesalia mahame kwani wengi wa wakazi wamelazimika kuyatoroka makazi yao kutokana na hali hiyo, kina mama na watoto wakiathirika pakubwa.
“Maeneo haya yamekuwa hatari sana hata watu wengi wamehama, wengine tumelazimika kuishi msituni. Na sasa kina mama na watoto ndio wanaoathirika sana na hali hii kwa sababu sasa hakuna chakula.” Walisema.
Wakazi hao walilalamikia kutelekezwa na serikali kwani baada ya kusalimisha silaha walizokuwa wakimiliki wamesalia bila mbinu yoyote ya kujilinda, huku wakilaumu hatua ya serikali kuwahami maafisa wa NPR wa upande wa Marakwet na kuwaacha wa upande wa Pokot magharibi.
“Waziri wa usalama alipokuja akapeana silaha upande mmoja na kuacha upande wa Pokot magharibi alifanya makosa. Alipasa kupeana silaha hizo pande zote siku iyo hiyo alipopeana upande wa Elgeyo marakwet. Sisi sasa hatuna jinsi ya kujilinda baada ya kusalimisha silaha zetu na sasa tunahangaishwa sana.” Walisema wakazi.
Walisema kwamba licha ya shule kufunguliwa nchini kwa muhula wa kwanza shule za eneo hilo zimesalia kufungwa wakitaka serikali kuchukua hatua za kuwatuma maafisa wa polisi kulinda shule ili angalau wanafunzi wa eneo hilo pia wapate kusoma kama wenzao wa maeneo mengine nchini.
“Shule zimesalia kufungwa kutokana na utovu wa usalama licha ya shule zingine nchini kufunguliwa. Tunataka serikali kutuma maafisa wa polisi kwa shule za eneo hili ili watoto wetu pia waweze kusoma jinsi ilivyo kwa maeneo mengine nchini.” Walisema.
Akizungumza afisini mwake mjini Kapenguria, kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam hata hivyo aliwahakikishia wakazi wa maeneo hayo kwamba maafisa zaidi wa polisi wametumwa eneo hilo kuimarisha doria pamoja na kutoa ulinzi kwa shule zote akiwahimiza wakazi kutohofu kuwapeleka wanao shuleni.
“Tunaendeleza oparesheni sehemu za Cheptulel, pokot ya kati na sehemu za pokot kusini. Na nawahakikishia wazazi wa maeneo haya kwamba hali ya usalama iko imara. Tumetuma maafisa zaidi kuhakikisha kwamba shule zote zinalindwa, kwa hivyo wazazi wasihofu kuwapeleka wanao shuleni.” Alisema Katam.