UTOVU WA USALAMA WAENDELEA KURIPITIWA KERIO VALLEY MWALIMU MMOJA AKIULIWA BARINGO.
Na Emmanuel Oyasi.
Hali ya taharuki imetanda eneo la Bartabwa, eneo bunge la Baringo kaskazini kufuatia kisa cha Jumapili wiki hii cha mauaji ya naibu mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Chemoe wenyeji wakikosa kuelewa lengo kuu la watu wanaoendeleza mauaji yanayoshuhudiwa eneo hilo.
Tukio hili limetokea juma moja tu baada ya mme, mkewe na mwanao mmoja kuuawa kinyama na majangili walipokuwa wakisafiri kwenda kujumuika na jamaa zao kwenye sherehe za kuwatoa watoto jandoni eneo la Chemoe katika kaunti ya Baringo, na kuwaacha waendeshaji wawili wa pikipiki na majeraha.
Wakizungumza na wanahabari, viongozi pamoja na wakazi kwenye eneo bunge hilo sasa wanaitaka serikali kuimarisha mikakati yake ya kuwakabili majangili hao ambao wamekuwa kero katika eneo zima la bonde la kerio kwa miaka mingi sasa.
“Hatutakubali kuendelea kuwapoteza watu wetu kiholela mikononi mwa wahalifu. Serikali inapasa kuweka mikakati ambayo itasaidia kuwaondoa wahalifu eneo hili. Kwa sababu ni kama oparesheni ya usalama inayoendelea haitatusaidia kwa vyovyote.” Walisema.
Haya yanajiri wakati rais william ruto amekariri azma ya serikali ya kukomesha ujambazi na wizi wa mifugo katika eneo la kaskazini mwa bonde la ufa.
Akizungumza katika ibaada ya jumapili mjini Itein kaunti ya Elgeyo Marakwet, rais alisrema serikali imepata vifaa vya kisasa kwa maafisa wa usalama kukabiliana vilivyo na majambazi.
“Tutamaliza mambo ya uhalifu eneo hili. Na watu wa kerio valley nawahakikishia kwamba tutakuwa na amani eneo hili. Na hii ni ahadi yangu kwamba tumejitolea kuwaondoa wahalifu hawa wanaowahangaisha wakazi.” Alisema rais Ruto.