UTEUZI WA LONYANGAPUO KUWA MWENYEKITI WA BODI YA MAJI KASKAZINI MWA BONDE LA UFA WAPONGEZWA.

Hatua ya rais William Ruto kumteua aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la ustawishaji wa maji eneo la kaskazini mwa bonde la ufa imeendelea kupongezwa na viongozi mbali mbali kaunti hyo.

Wa hivi punde kupongeza uteuzi huo ni mwakilishi wadi mteule Bruno Lomeno ambaye alisema hatua hiyo ni heshima kuu ya utawala wa rais William Ruto kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi ambao wametengwa kwa miaka mingi na serikali zilizotangulia.

“Tunapongeza sana kuteuliwa kwa aliyekuwa gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo kusimamia bodi ya maji eneo la north rift. Hii inaonyesha kwamba rais William Ruto anajali sana jamii ya Pokot baada ya kutengwa sana katika serikali zilizotangulia.” Alisema Bruno.

Bruno alitoa wito kwa Lonyangapuo kutumia fursa hiyo kuhakikisha kwamba tatizo la maji ambalo limekumba maeneo mengi ya kaunti hiyo kwa miaka mingi linapata suluhu ya kudumu na kutia kikomo kwa mahangaiko ya wakazi kutafuta bidhaa hiyo muhimu.

“Tunataka sasa Lonyangapuo afanye kazi. Hii kaunti ina tatizo kubwa la maji na sasa tunatarajia kwamba atumie nafasi hii kuhakikisha kwamba wananchi wa kaunti hii hawapati tena tatizo la kupata maji safi ya matumizi.” Alisema.

Wakati uo huo Bruno alisema shule nyingi za kaunti hiyo zinakabiliwa na changamoto ya maji akidokeza kwamba kama viongozi wanaendelea kushirikiana na serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba changamoto hiyo inashughulikiwa.

“Bado tuna tatizo la maji katika shule zetu. Na sisi kama viongozi tutashirikiana kikamilifu na serikali kuhakikisha kwamba maji yanafikia shule za kaunti hii ili kuwapa watoto nafasi bora ya kuendeleza masomo na kutotumia muda mwingi kutafuta maji.” Alisema.