UTEUZI WA JOEL ARUMONYANG KAMA KATIBU WAENDELEA KUVUTIA HISIA POKOT MAGHARIBI.


Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepongeza uteuzi wa rais William Ruto wa makatibu katika wizara mbali mbali za serikali yake.
Kachapin aidha alipongeza uteuzi wa Joel Arumonyang kuwa katibu katika  idara ya kazi za umma chini ya wizara ya ardhi, kazi za umma, nyumba na maendeleo ya miji.
Kachapin alisema uteuzi wa Arumonyang katika idara hiyo ni dhihirisho si tu la upendo wake rais Ruto kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi, bali pia imani yake kwa uwezo wao wa kumsaidia kufanikisha ahadi alizotoa kwa wakenya.
Aidha wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wakiongozwa na mwanaharakati Peter Lomada walisema kwamba hatua hiyo ya rais Ruto ni tunuku kuu kwa wakazi wa kaunti hii ambao walijitokeza kwa wingi kumpigia kura katika uchaguzi mkuu wa agosti 9.
“Tunampongeza rais wa jamhuri ya Kenya William Ruto kwa kumteua Joel Arumonyang. Hii ni tunuku kubwa kwa wakazi wa kaunti hii ambao walimpelekea kupata ushindi wa urais. Sasa ni jukumu la wakazi wa kaunti hii kuunga mkono uteuzi huo.” Alisema Lomada.
Wakati uo huo Lomada alimtaka Arumonyang kuandaa kikao na wazee wa kaunti hii ili wampe mwelekeo wa jinsi ya kutekeleza majukumu yake huku pia akimtaka kutumia fursa hiyo kuwatafutia ajira vijana wa kaunti hii.
“Namwomba Arumonyang kwamba aje aketi na wazee ili wamwelekeze vizuri jinsi ya kutekeleza majukumu yake. Namwomba pia atumie fursa hiyo kuwatafutia nafasi za ajira watoto wetu katika kaunti hii ya Pokot magharibi.” Alisema.