UTAPIA MLO WATAJWA KUKITHIRI POKOT MAGHARIBI MASHIRIKA YA KIJAMII YAKICHANGIA JUHUDU ZA KUKABILI HALI HIYO.


Shirika la Action Agaisnt Hunger ACF limeikabidhi hospitali ya kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi dawa zitakazotumika kuwashughulikia watoto walioathirika na utapia mlo maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo.
Akizungumza wakati akipokezwa dawa hizo zilizogharimu zaidi ya shilingi milioni 7, waziri wa afya kaunti hiyo Cleah Parklea alipongeza shirika hilo akisema kwamba maeneo yaliyoathirika zaidi hasa pokot ya kati, pokot ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya pokot kusini ndiyo yatakayopewa kipau mbele katika usambazaji wa dawa hizo.
“Tunafahamu kaunti yetu inakabiliwa na baa la njaa na wanaoumia zaidi ni kina mama na watoto. ACF wameona ni vyema kuja mapema. Tutayapa kipau mbele maeneo ambayo yameathirika zaidi hasa Pokot ya kati, Pokot kaskazini na baadhi ya maeneo ya pokot kusini katika usambazaji wa dawa hizo.” Alisema Parklea.
Kulingana na afisa anayesimamia lishe bora katika kaunti hii ya Pokot magharibi Leah Chelobei, kati ya kila watoto 100 katika kaunti hii, 20 wameathirika na utapia mlo, akisema kwamba msaada huo kutoka kwa ACF utasaidia katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo.
“Kati ya watoto 100 miongoni mwao 20 wana tatizo la utapia mlo. Na msaada huu wa ACF utasaidia zaidi katika juhudi zetu za kuhakikisha kwamba visa vya utapia mlo vinapungua katika kaunti hii.” Alisema Parklea.
Kwa upande wake afisa katika shirika hilo la ACF Salome Tsindori alisema kwamba walilazimika kushirikiana na serikali ya kaunti kupitia kutoa dawa hizo kutokana na idadi kubwa ya watoto ambao wanakumbwa na utapia mlo kulingana na utafiti ulioendeshwa na shirika hilo.
“Tuna utafiti tuliofanya na tukabaini kuwa karibu asilimia 15 ya watoto chini ya miaka 5 wana utapia mlo. Na hii ndiyo sababu tuliamua kama shirika kushirikiana na serikali ya kaunti kutafuta wafadhili ambao wataingilia kati ili hawa watoto wapate matibabu yanayofaa.” Alisema Tsindori.