USHIRIKIANO MIONGONI MWA RAIA NA POLISI BONDE LA KERIO WATAJWA KUCHANGIA KUPUNGUA UHALIFU.
Mbunge wa Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto amepongeza ushirikiano uliopo baina ya raia na maafisa wa usalama katika kaunti hiyo hasa maeneo ya mipakani ambapo kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama.
Akizungumza baada ya kikao cha kuangazia hali ya usalama Moroto alisema kwamba ushirikiano huo umepelekea kupungua pakubwa visa vya uvamizi katika siku za hivi karibuni maeneo mengi ya bonde la Kerio.
Moroto alitumia fursa hiyo kuwasuta baadhi ya viongozi wa serikali kuu hasa katika idara ya usalama kwa kile alisema kwamba kutoa maagizo kuhusu hali ya usalama eneo hilo badala ya kufika wenyewe kuona jinsi hali ilivyo kuhusiana na swala zima la usalama.
“Visa vya uvamizi unaotekelezwa na wahalifu vimepungua eneo hili la bonde la kerio kutokana na ushirikiano ambao umekuwepo baina ya raia na maafisa wa polisi. Na tunaomba hili liendelee ili tuwakabili watu wachache ambao wamekuwa wakiwahangaisha watu wetu.” Alisema Moroto.
Wakati uo huo Moroto aliilaumu katiba ya sasa kuwa chanzo cha kuendelea kushuhudiwa uhalifu nchini kutokana na hali kuwa inaruhusu wanaopatikana kutekeleza uhalifu kuachiliwa kwa dhamana, akisema kwamba hawafai kuruhusiwa kutangamana na wananchi.
“Hii katiba ya sasa ndio mbaya kabisa kwa sababu inaruhusu watu ambao wanakamatwa kuhusika mauaji ya watu wengi kuachiliwa kwa dhamana. Hawa si watu wa kuwachiliwa kwa sababu wakifika huku nje wanaanza kusema sasa nimetoka na wanaendelea kuwahangaisha wananchi.” Alisema.
Ni kauli iliyotiliwa mkazo na aliyekuwa waziri katika serikali iliyotangulia Francis Kitalauyan ambaye aidha aliwataka maafisa wa idara ya DCI kumakinika katika majukumu yao na kuhakikisha wanaotekeleza uhalifu wanafuatiliwa na kuchukuliwa hatua.
“Tunawataka hawa watu wa DCI kutekeleza vyema majukumu yao ya kufuatilia kwa kina wahalifu hawa na kuhakikisha kwamba wanapatikana na kuwachukulia hatua. Kazi yao si kuanza kulazimisha wananchi kuzungumza kuhusiana na hawa watu.” Alisema Kitalauyan.