USHINDI WA RUTO WAENDELEA KUSHEREHEKEWA KOTE NCHINI.
Baadhi ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi ambao ni wafuasi wa muungano wa Kenya kwanza wameendelea kupongeza uamuzi wa mahakama ya juu uliodumisha ushindi wa rais Mteule William Ruto.
Wakiongozwa na Abraham Tukomoi wakazi hao wamesema uamuzi huo wa jopo la majaji saba wa mahakama ya juu ni dhihirisho tosha kwamba Ruto alishinda uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi agosti kwa njia huru na iliyo ya haki.
Wakazi hao wameelezea imani kwamba taifa litaimarika chini ya uongozi wa Ruto hasa ikizingatiwa rekodi yake ya maendeleo katika kipindi ambacho amehudumu serikalini.
Wakati uo huo wakazi hao wamepongeza jopo la majaji saba wa mahakama ya juu wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome wakisema kuwa majaji hao wamedhihirisha wazi kwamba mahakama ni idara huru ambayo haiwezi kushawishiwa na yeyote.
Uamuzi huo wa Mahakam pia ulipongezwa na viongozi katika kaunti ya Trans nzoia wakiongozwa na mwakilishi wadi mteule wa wadi ya Sitatunga eneo la Cherang’ani Simon Murei, na ambao walisema kuwa uamuzi huo sasa unaimarisha imani ya wakenya katika idara ya mahakama katika utendaji haki.
Murei aidha aliwataka viongozi wanaoegemea mrengo wa azimio kukubali uamuzi huo wa mahakama na kutoa nafasi kwa serikali ya William Ruto kuwatekelezea wakenya maendeleo.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwakilishi wadi mteule wa wadi ya Kinyoro Andrew Kibet Kipekee ambaye aidha amewataka wapinzani wa ruto kumheshimu kwani ndiye sasa rais wa taifa hili.