USAJILI WAWANAOJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA WASHUHUDIA IDADI KUBWA.


Usajili wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza ukiingia leo siku ya tatu, wakuu wa shule mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamesema kuwa zoezi hilo linaendelea vyema huku kanuni za kukabili maambukizi ya virusi vya corona zikizingatia katika zoezi zima.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Mnagei Ann Lotuliatum amesema kuwa katika siku ya kwanza pekee shule hiyo iliyotengewa nafasi 168 za wanafunzi iliweza kusajili wanafunzi 98 huku akielezea matumaini ya kusajili zaidi ya idadi iliyotengewa shule hiyo.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Nasokol Suzan Obiri ambaye ameelezea hofu kuwa huenda wakalazimika kubuni nafasi zaidi kwa ajili ya idadi kubwa ya wanafunzi ambao wanatarajiwa kujiunga na shule hiyo kufikia mwisho wa zoezi la usajili kwani madarasa yaliyopo kwa sasa hayatoshelezi mahitaji.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Chewoyet Kiminisi Barasa amelalamikia changamoto ya ulipaji wa karo miongoni mwa wazazi wanaowapelekea wanao shuleni hali anayosema imetokana na kubadilishwa kalenda ya masomo kutokana na athari za janga la corona.