URAIBU WA POMBE NA DAWA ZA KULEVYA WATISHIA MUSTAKABALI WA VIJANA MATHARE, POKOT MAGHARIBI.

Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia idara za usalama imetakiwa kuingilia kati na kukabili matumizi ya dawa za kulevya na pombe katika mtaa wa mathare viungani mwa mji wa makutano ambayo yametajwa kukithiri kwenye mtaa huo.

Akizungumza na kituo hiki mwenyekiti wa mpango wa nyumba kumi katika mtaa huo Bonface Ayuma alisema kwamba visa vya utovu wa usalama vimeongezeka katika mtaa huo kufuatia uraibu huo ambao umetajwa kukolea miongoni mwa vijana na hata kina mama.

“Tuna changamoto kubwa sana katika kijiji cha Mathare kutokana na kukithiri ulevi na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na hata kina mama. Vijana wengi wanafanya uhalifu kwa sababu ya kutumia dawa za kulevya.” Alisema Ayuma.

Ayuma alisema kwamba imekuwa vigumu kwake na wazee wa mitaa kukabiliana na visa hivyo kutokana na hali kwamba wanaonaswa na maafisa wa polisi kufuatia uraibu huo huachiliwa muda mfupi baadaye bila kuchukuliwa hatua zozote.

“Cha kushangaza ni kwamba tunaporipoti mambo kama haya, vijana hawa wanakamatwa  na polisi ila baadaye wanaachiliwa baada kipindi kifupi sana bila hata kuchukuliwa hatua. Hali hii imewatia kiburi hata kuwafanya kufanya mambo haya hadharani.” Alisema.

Ayuma alisema kwamba uraibu huo haujawasaza hata wanafunzi akitoa wito kwa wazazi eneo hilo kuwa makini na wanao na kufuatilia mienendo yao na kuhakikisha kwamba wanaelekea shuleni moja kwa moja wanapotoka nyumbani ili kuhifadhi kizazi kijacho.

“Kuna wakati nimefukuzana na wanafunzi hapa. Wana marafiki ambako wanaacha nguo za nyumbani wanapoelekea shuleni ambapo wakitoka shuleni baadaye wanavaa hizo nguo na kujihusisha na uhalifu. Naomba wazazi wafuatilie mienendo ya wanao.” Alisema.