UPANGAJI UZAZI WAKUMBATIWA NA ASILIMIA KUBWA POKOT MAGHARIBI.
Takwimu za hivi punde zinaashiria kwamba asilimia kubwa ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi sasa wamekumbatia mbinu za kupanga uzazi.
Akizungumza na wanahabari baada ya kikao cha kutoa matokeo ya utafiti uliofanywa na idara ya afya kaunti hii kuhusu matumizi ya mbinu hizo, mshirikishi wa afya ya uzazi kaunti hii Wilson Ng’aren amesema kuwa kwa sasa ni asilimia 33 ya wakazi wanaotumia mbinu hizo ikilinganishwa na asilimia 14 miaka mitatu iliyopita.
Aidha Ng’aren amesema kuwa uhamasisho ambao umekuwa ukiendeshwa na idara hiyo umepelekea kupungua mimba za mapema miongoni mwa watoto wa kike kaunti hii kutokana na hali kwamba wengi wa vijana wanatumia mbinu salama wakati wakishiriki ngono.
Wakati uo huo amesema mpango huo unaendelezwa hadi kwa watu wenye ulemavu ambapo wahudumu wa afya wamechukua jukumu la kuyafikia makundi hayo ili kuhakikisha kuwa nao wananufaika na huduma hizo sawa na wakenya wengine.