UONGOZI WA SHULE YA KAPKECHO WASHUTUMIWA KWA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA.


Wazazi wa shule ya upili ya Kapkecho eneo la Siyoi katika kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu uongozi wa shule hiyo kwa kile wamedai usimamizi mbaya huku wakitaka mwalimu mkuu wa shule hiyo kupewa uhamisho.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao John Saisi wazazi hao wamemshutumu mwalimu mkuu wa shule hiyo Samson Chemweru kwa madai ya matumizi mabaya ya fedha wakidai kuwa mwalimu huyo kwa ushirikiano na kamati simamizi ya shule wamekuwa na mazoea ya kutumia fedha za shule bila mipangilio hitajika.
Aidha wazazi hao wamemshutumu mwalimu huyo kwa kuchangia matokeo duni katika kipindi ambacho imefanya mitihani ya kitaifa, hali ambayo wamesema imechochewa na utepetevu wake katika kuhakikisha walimu wanahudhuria vipindi vya masomo, wakimtaka kuondoka katika shule hiyo.
Hata hivyo mwalimu huyo Samson Chemweru amepuuzilia mbali madai dhidi yake akilaumu bodi ya shule hiyo chini ya mwenyekiti Wilson Lonyang’ole ambaye amedai amedinda kushirikiana naye katika kutafuta suluhu kwa matatizo yanayokumba shule hiyo.
Juhudi za kutafuta kauli kutoka kwa mwenyekiti huyo zimeambulia patupu baada yake kudinda kuzungumza na wanahabari.
Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa mwalimu huyo kuhusishwa katika sakata ya matumizi mabaya fedha.

[wp_radio_player]