UNYANYAPAA NA TAMADUNI VYATAJWA KUWA VIKWAZO VYA HUDUMA BORA KWA WALEMAVU POKOT MAGHARIBI.

Jamii imetakiwa kuhusika katika uhamasishaji dhidi ya unyanyapaa unaotelekezwa dhidi ya watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Pokot magharibi.

Ni wito wake mkewe gavana wa kaunti hiyo Sofia Kachapin ambaye alisema kwamba unyanyapaa dhidi ya watu hao pamoja na tamaduni vimekuwa vikwazo vikuu katika kuwasajili watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti hii.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya walemavu duniani iliyoandaliwa eneo la Alale Bi. Kachapin alisema kati ya watu alfu 93,150 wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo ni walemavu alfu 7,928 pekee ambao wamesajiliwa.

“Kati ya idadi yote ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi watu alfu 93,150 ni watu wanaoishi na ulemavu ila kati ya hawa ni watu alfu 7,928 pekee ambao wamesajiliwa na baraza la kitaifa. Utamaduni na unyanyapaa umekuwa kikwazo kikubwa katika usajili wa walemavu kaunti hii.” Alisema Sofia.

Kwa upande wake naibu kamishina eneo la pokot kaskazini Mourice Ogweno aliilaumu jamii kwa kuwabagua watoto wanaoishi na ulemavu akisema kwamba kuanzia mwaka ujao vitengo vya usalama vitaendesha opareseni ya kuhakikisha watoto wote wanahudhuria masomo haijalishi hali yao.

“Watoto wanaoishi na ulemavu katika kaunti hii wanabaguliwa sana na jamii. Ila sisi kama serikali ya kitaifa tuna amri ya kuhakikisha kwamba kuanzia mwaka ujao watoto wote ambao hawaendi shule wanahudhuria masomo.” Alisema Ogweno.