UNICEF YAHIMIZA MDAHALO KUHUSU AFYA YA WATOTO KUPEWA KIPAU MBELE.

Shirika la kushighulikia mswala ya watoto UNICEF limeelezea haja ya wadau kuendeleza mdahalo kuhusiana na maswala yanayowapa kipau mbele watoto kaunti ya Pokot magharibi ili kuwepo na mbinu mpya za ubunifu pamoja na mipango ya kuhakikisha kwamba watoto wanapata mahitaji ya kimsingi inavyohitajika.

Aikiongoza ujumbe wa UNICEF katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi, naibu mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika mashariki na kusini, Lieke Von de Wiel alisema kwamba hali ilivyo sasa watoto wanapitia changamoto kupata mahitaji ya kimsingi kufuatia athari zilizosababishwa na janga la Covid 19 pamoja na ukame unaoshuhudiwa .

“Hatua kadhaa zilipigwa katika miaka iliyopita ila kufuatia janga la covid 19 na mwaswala ya ukame, imekuwa changamoto kuendelea kupiga hatua. Hii ndiyo sababu inapasa wadau kuendeleza mdahalo kuhusiana na mwaswala ya kuwapa kipau mbele watoto.” Alisema Wiel.

Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin ambaye ni mwenyeji ujumbe huo alisema kwamba kaunti hiyo haijaafikia viwango hitajika katika kuhakikisha afya ya watoto pamoja na akina mama wanaojifungua na kwamba ushirikiano na shirika hilo ni muhimu katika kuhakikisha hali hii inashughulikiwa.

“Kama kaunti hatufanyi vyema kuhusiana na maswala ya afya ya watoto pamoja na vifaa vya kujifungua kina mama. Hivyo ushirikiano huu kati ya kaunti na shirika la UNICEF ni muhimu sana na kama kaunti tutashirikiana kikamilifu na shirika hilo kuhakikisha kwamba tunaafikia malengo hitajika.” Alisema Kachapin.

Ni kauli ambayo ilikaririwa na waziri wa afya katika kaunti hiyo Cleah Parklea ambaye aidha alisema  shirika hilo limekuwa la manufaa zaidi katika kaunti hiyo kufuatia miradi mingi ambayo linatekeleza ikiwemo elimu na afya.

“UNICEF inafanya kazi nzuri sana kaunti hii ya Pokot magharibi, na kuna miradi mingi sana ambayo linaendeleza kuwafaa wakazi hasa katika sekta ya elimu na afya.” Alisema Parklea.