UMASIKINI MIONGONI MWA KINA MAMA WATAJWA KUWA CHANZO CHA DHULUMA ZA KIJINSIA POKOT MAGHARIBI.
Umasikini miongoni mwa kina mama ni miongoni mwa maswala ambayo yametajwa kuwa vyanzo vikuu vya dhuluma za kijinsia katika jamii kaunti ya Pokot magharibi kwenye mafunzo ambayo yanatolewa kwa akina mama kuhusu jinsi ya kujiwezesha kiuchumi na shirika moja lisilo la serikali kaunti hiyo.
Akizungumza kwenye mkahawa mmoja mjini Makutano wakati wa kutoa mafunzo hayo, afisa wa fedha na ujasiriamali katika shirika la collaborative centre for gender and development Maureen Wairimu, alielezea haja ya kina mama kuwezeshwa kiuchumi ili wasiwe wa kutegemea zaidi waume zao kwa kila jambo na kuishia kudhulumiwa.
“Kazi kubwa ambayo tunafanya katika shirika hili ni kuhamasisha jamii kujitenga na dhuluma za kijinsia. Na tumetambua kwamba dhuluma nyingi dhidi ya kina mama zinatokana na umasikini miongoni mwao hali ambayo inawafanya kuwategemea zaidi waume zao.” Alisema Wairimu.
Kauli yake ilisisitizwa na afisa katika shirika hilo Irene Cheruto ambaye alisema kwamba mafunzo haya yamesaidia vile vile katika kupunguza pakubwa visa vya ukeketaji kaunti hiyo, hasa msimu huu ambao ndio huripoti visa vingi, akitoa wito kwa jamii kujitenga na tamaduni hii ambayo amesema ni dhuluma kubwa kwa mtoto wa kike.
“Tunafurahia kwa sababu mafunzo haya yamesaidia pakubwa katika kupunguza baadhi ya dhuluma kama vile ukeketaji. Hivyo nahimiza jamii kwamba tuendeleze uhamasisho kuhusu athari za ukeketaji.” Alisema Cheruto.
Kina mama ambao wamehudhuria mafunzo hayo wameelezea umuhimu wake wakisifia shirika hilo kwa ufahamu ambao wamesema kwamba umewapa mwanga zaidi kuhusiana na athari za dhuluma za jinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za mapema kwa wanao wa kike.
“Tunashukuru kwa haya mafunzo kwa sababu tumeweza sasa kufahamu madhara ya kuendeleza tamaduni ya ukeketaji. Na pia tumefahamu umuhimu wa kuwapa watoto wa kike nafasi ya kusoma badala ya kuozwa mapema.” Walisema.