Ukosefu wa sheria za misitu ndicho chanzo cha uharibifu wa mazingira

Msitu wa Kamatira Kaunti Ya Pokot Magharibi,Picha/Maktaba

Na Benson Aswani,
Idara ya mazingira na mali asili katika kaunti ya Pokot magharibi imetaja ukosefu wa sheria za kulinda mazingira dhidi ya uharibifu kuwa chanzo cha kukithiri uharibifu wa mazingira unaoendelezwa na binadamu.


Akizungumza na kituo hiki afisa katika idara hiyo Kenneth Kariwo alisema kwamba ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya uchomaji makaa umekithiri katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi, kutokana na ukosefu wa sheria thabiti za kulinda mazingira.


“Hatujazingatia inavyofaa mazingira yetu katika kaunti hii kutokana na ukosefu wa sheria za kutunza mazingira. Tukiwa na sheria, zitatusaidia kudhibiti hata shughuli ya ukataji miti kwa ajili ya kuchoma makaa,” alisema Kariwo.


Hata hivyo Kariwo alisema kwamba kwa ushirikiano na wadau wengine idara hiyo inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba sheria za mazingira zinabuniwa katika juhudi za kuhakikisha mazingira yanatunzwa.


“Kwa sasa tunashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kwamba kuna sheria ambazo zitasaidia katika kuhakikisha mazingira yetu yanalindwa,” alisema.


Kwa upande wake naibu mkurugenzi katika idara hiyo Raphael Magal aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuhakikisha wanatumia msimu huu wa mvua kupanda miti kwa wingi katika mashamba yao, na pia kujizuia na hulka ya ukataji miti kiholeloa.


“Nawahimiza wakazi katika kaunti hii wakumbatie zoezi la upanzi wa miti msimu huu wa mvua ili tuongeze viwango vya misitu. Tunapasa pia kukoma hulka ya ukataji miti kiholela na tutunze misitu yetu,” alisema Magal.