UKOSEFU WA MADAKTARI MARICH WA WAFANYA WANANCHI KUTEMBEA MWENDO MREFU KUTAFTA HUDUMA
Wakazi wa eneo la Marich Sigor katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia huduma duni za afya kufuatia ukosefu wa madaktari katika kituo cha afya eneo hilo kwa takriban miaka mitano sasa.
Wakazi hao wamesema kwamba wanalazimika kusafiri kwa mwendo mrefu hadi eneo la Sigor kutafuta huduma hizo, masaibu yao yakizidishwa na makali ya njaa ambayo yamekithiri huku wengine wakilazimika kutembea kwa miguu kutafuta huduma hizo.
Aidha wakazi hao wamelalamika kwamba kina mama wajawazito wanapitia hali ngumu wakilazimika kujifungulia barabarani katika harakati za kutafuta huduma za madaktari wakitoa wito kwa serikali ya kaunti kuchukua hatua za haraka kuwashughulikia.
Wakazi hao pia wamelalamikia uhaba wa maji hali ambayo imeathiri huduma za afya na shughuli za masomo katika shule za eneo hilo wakisema kuwa wanalazimika kutegemea kisima kimoja tu na hata wengine kutumia maji ya mtoni ambayo hata hivyo si salama.