UKOSEFU WA ELIMU MIONGONI MWA WAKAZI WATAJWA KUWA CHANZO CHA UTOVU WA USALAMA KERIO VALLEY.
Mbunge wa sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ametoa wito kwa serikali kuwekeza raslimali nyingi eneo hilo analosema kwamba lingali nyuma zaidi kimasomo ikilinganishwa na maeneo mengine ya kaunti hyo.
Lochakapong alisema kwamba visa vya utovu wa usalama ambavyo vinashuhudiwa eneo hilo kufuatia wizi wa mifugo vinatokana na hali kwamba idadi kubwa ya wakazi hawajapata elimu, akielezea haja ya kujengwa miundo msingi ya kutosha ikiwemo shule na barabara ili kuafikiwa hilo.
“Idadi kubwa ya wakazi wa sigor hawajapata elimu hali ambayo imechangia pakubwa visa vya wizi wa mifugo. Kwa hivyo naomba katika huu mpango wa serikali tuangazie sehemu kama hiyo ili tuweke raslimali nyingi kwa ujenzi wa shule, barabara na hata ikiwezekana watoto wa eneo hilo wasome bure.” Alisema Lochakapong.
Na siku moja tu baada waziri wa usalama Prof. Kithure Kindiki kuwaagiza wakazi wa maeneo yanayoshuhudia utovu wa usalama kuondoka ili kupisha awamu ya pili ya oparesheni hiyo, Lochakapong alitaka shughuli hiyo kuendeshwa kwa kuheshimu haki za binadamu wala isiwe ya kuwahangaisha.
“Tunakubali oparesheni ambayo inaendelea bonde la kerio ila oparesheni hiyo inafaa kufanyika katika njia ambayo inaheshimu haki za binadam. Wanaoendeleza opareseheni hiyo wasitumie fursa hiyo kuwahangaisha wakazi.” Alisema.
Wakati uo huo Lochakapong alielezea imani kwamba serikali ya rais William Ruto itawakabili wahalifu hao ambao wamewahangaisha wakazi kwa miaka mingi katika bonde la kerio, akisema itakuwa bora iwapo hilo litaafikiwa ili kupisha safari ya maendeleo maeneo husika.
“Nina uhakikika kwamba rais atatatua tatizo hili la usalama kerio valley jinsi alivyosema. Na hatua hiyo itakuwa bora kabisa kwani sasa itafungua safari ya kuafikiwa maendeleo eneo hili.” Alisema.