UKEKETAJI WASALIA CHANGAMOTO KATIKA BAADHI YA MAENEO POKOT MAGHARIBI.

Chifu wa eneo la yanglomu Lomut kaunti hii ya Pokot magharibi Yohana Loritai amelalamikia kukithiri visa vya ukeketaji wa watoto wa kike licha ya juhudi za serikali na mashirika mbali mbali ya kijamii kuhakikisha visa hivyo vinamalizwa kaunti hii.

Loritai alisema kwamba visa hivyo hukithiri zaidi nyakati za likizo wanafunzi wakiwa nyumbani, ambapo baadhi ya wazazi huviendeleza kisiri baada ya kubaini huenda wakabiliwa vikali kisheria  iwapo watapatikana.

Chifu huyo sasa anapendekeza kuwepo na vituo vya kuwahifadhi watoto wa kike wakati shule zinapofungwa kwa likizo na kuwalinda dhidi ya kutendewa uovu huo ili wapate nafasi bora ya kuendeleza masomo na kuafikia ndoto zao maishani.

“Wakati wa likizo watoto wa kike eneo hili wanapitia ukatili wa ukeketaji. Kama idara ya usalama tunang’ang’ana kwa ushirikiano na mashirik mbali mbali kutia kikomo tamaduni hii lakini wapo wale ambao wanaendeleza tabia hii kisiri. Ingekuwa bora kama tungekuwa na vituo ambavyo watoto hawa wangekaa wakati wa likizo ili kuzuia haya.” Alisema Loritai.

Wakati uo huo Loritai alitaja umasikini na njaa miongoni mwa familia nyingi eneo hilo kuwa changamoto kuu kwa elimu ambapo wazazi wengi wanapata ugumu wa kuwapeleka wanao shuleni akitaka hatua za dharura kuchukuliwa na wadau husika ili kuinusuru jamii.

“Changamoto kuu ambayo inatukabili hapa ni umasikini na njaa. Haya yameathiri pakubwa elimu eneo hili kwani imekuwa vigumu kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shule.” Alisema.

[wp_radio_player]