UKEKETAJI WA WASALIA KIZUNGUMKUTI POKOT MAGHARIBI.


Visa vya ukeketaji vimesalia changamoto kuu katika kaunti nyingi za wafugaji hali ambayo mashirika ya haki za wanawake yametaja kuwa inatokana na ukosefu wa elimu miongoni mwa wakazi wengi wa kaunti hizi.
Kulingana na mashirika hayo kando na tamaduni hizi zilizopitwa na wakati, watoto wa kike na wanawake kwa jumla katika kaunti hizi hawana ufahamu kuhusu haki zao hali inayolemaza juhudi za kukabiliana na dhuluma za kijinsia.
Kaunti hii ya Pokot magharibi kwa mfano ina asilimia 6.8 ya visa hivyo ikilinganishwa na asilimia 9.2 ya visa hivyo kitaifa kulingana na utafiti uliofanywa kituo cha kitaifa cha utafiti wa uhalifu National Crime Research Centre mwaka 2018.
Kulingana na mkurugenzi wa wakfu wa IREP Foundation Domtila Chesang, wengi wanaoendeleza dhuluma za kijinsia hawachukuliwi hatua hali ambayo imeathiri pakubwa vita dhidi ya visa hivi katika kaunti hii.
Akizungamza katika mkutano wa kina mama eneo la Kongelai kaunti hii ya Pokot magharibi, Chesang alisema dhuluma hizi zimewafanya wanawake na wasichana kuwa watumwa huku wengi wakiamini kwamba sauti zao haziwezi kusikika.
Aidha wakfu huo ulifichua kuwa asilimia 67 ya wakazi wa kaunti hii hawana elimu huku idadi kubwa ikiwa wanawake.
“idadi ya wanafunzi shuleni ni ya chini mno kwa sasababu watoto wa kike hulazimika kuolewa katika umri mdogo zaidi. Serikali inapasa kuchukua hatua za dharura kujenga vituo vya kuwaokoa wasichana ili kuwalinda dhidi ya ndoa za mapema.” Chesang alisema.
Wakati uo huo Chesang alitoa wito kwa jamii kujitenga na tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema ambazo zimezidi kuwa pigo kwa mtoto wa kike.
“Tunataka wanawake na wasichana kufurahia haki sawa. Tunahitaji kuhamasisha jamii kuwalinda wanawake dhidi ya tamaduni dhalimu.” Alisema.
Aliongeza kwamba tamaduni hizi haziwezi kufika kikomo iwapo wanawake hawataelimishwa kuhusu haki zao, akiongeza kuwa wanawake wanapasa kuunda makundi yatakayowasaidia kupata raslimali za kujiwezesha.