UKEKETAJI NA NDOA ZA MAPEMA ZASALIA CHANGAMOTO KWA MTOTO WA KIKE POKOT MAGHARIBI.
Swala la ukeketaji na ndoa za mapema limesalia changamoto kuu kwa mtoto wa kike katika kaunti ya Pokot magharibi.
Akizungumza eneo la Kamula wadi ya Kiwawa, mkurugenzi wa idara ya watoto kaunti ya Pokot magharibi Philip wapopa alisema hali hii imeathiri pakubwa nafasi ya mtoto wa kike katika jamii, na hata kuchangia kukithiri visa vya utapia mlo miongoni mwa watoto kufuatia hali kwamba wasichana wengi wanaoozwa wanajifungua katika umri ambao ni vigumu kuwalea wanao.
“Hapa kwetu mtoto wa kike ameathirika sana na maswala ya ukeketaji na ndoa za mapema. Na ndio maana tunaona visa vingi vya utapia mlo kwa sababu wasichana ambao wanaozwa wanashindwa jinsi ya kuwalea wanao wanapojifungua, kutokana na hali kwamba hawajafika ule umri wa kufahamu anachohitaji mtoto.” Alisema Wapopa.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na msaidizi wa kamishina katika wadi ya Kiwawa Nimrod Kane, ambaye alisema kwamba hali hii imepelekea wengi wa watoto wasichana kukosa kuafikia ndoto zao maishani kwani wengi wao hawapati nafasi ya kupata elimu.
“Mtoto msichana katika kaunti hii ana changamoto nyingi sana kwa sababu wengi wao hawapati nafasi ya kuendeleza elimu yao kutokana na tamaduni ambazo zinaendelezwa na jamii.” Alisema Kane.
Mshirikishi wa miradi katika shirika la kijamii la umoja development organization Ambrose Merian alisema shirika hillo linaendeleza miradi mbali mbali ambayo inalenga kuhakikisha kwamba mtoto wa kike anaheshimika katika jamii.
“Tunaendeleza mipango mbali mbali ya kuwahusisha wakazi hasa wale ambao wameasi tamaduni hii ya ukeketaji, ambao wanahudumu kama macho yetu kwa jamii ili kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa haraka kuzuia ukeketaji ambao unapangwa kufanyika.” Alisema Merian.
Kwa upande wao wadau katika sekta ya elimu kaunti hiyo wametoa wito kwa wazazi kufahamu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kutimiza ndoto yake maishani.
“Tunatoa wito kwa wazazi kwamba wazingatie elimu kwa wanao kwani ni muhimu sana kwa maisha yao ya baadaye. Wawape watoto wa kike nafasi ya kupata elimu ili nao waweze kutimiza ndoto zao maishani.” Walisema.