UKAME UNAOSHUHUDIWA POKOT KASKAZINI WATAJWA KUWA CHANZO CHA NDOA ZA MAPEMA.

Swala la ndoa za mapema na ukeketaji miongoni mwa watoto wa kike limesalia kuwa changamoto kuu kwa elimu ya mtoto wa kike katika kaunti ya Pokot magharibi eneo la pokot kaskazini likitajwa kuwa lilioathirika zaidi na visa hivyo.

Akizungumza baada ya kikao na wadau mbali mbali kuhusu swala hilo, balozi wa amani ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake Julia Lobron alisema kwamba hali hii inasababishwa na ukame ambapo wengi wa wazazi wanawaoza wanao ili wapate ng’ombe watakaouza ili kujikimu kimaisha.

“Mtoto msichana ameathirika sana eneo hili la pokot kaskazini. Na mara nyingi visa hivi vya kuozwa mapema husababishwa na hali ya ukame ambapo wazazi wanawaoza wanao ili kupata mifugo  watakaowauza ndipo wapate jinsi ya kujikimu kimaisha.” Alisema Lobron.

Wadau mbali mbali waliohudhuria kikao hicho kilichoandaliwa eneo la Kacheliba walitoa wito kwa wazazi kujitenga na tamaduni hizo zilizopitwa na wakati na badala yake kuwapa nafasi ya kupata elimu wanao ili kutimiza ndoto zao maishani.

“Natoa wito kwa wananchi hasa wakazi wa eneo hili kujitenga na hii tamaduni dhalimu ya kuwakeketa na kuwaoza watoto wa kike ili angalau nao wapate fursa ya kusoma na kuafikia ndoto zao maishani kama wenzao wa kiume.” Walisema.

Kwa upande wake OCS wa Kacheliba Tom Nyanaro alielezea hofu kwamba huenda baadhi ya wazazi wakatumia fursa ambapo watoto wako nyumbani kwa likizo fupi kuwaoza au kuwakeketa akisema  kwa ushirikiano na wadau mbali mbali watahakikisha kwamba kila mtoto anarejea shuleni akiwa salama.

Mara nyingi wazazi hutumia fursa ambapo watoto wapo nyumbani kuwaoza. Lakini sasa tumeelewana na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba kila mtoto anarejea shuleni akiwa katika hali nzuri jinsi alivyokuja nyumbani.” Alisema Nyanaro.