UHABA WA LISHE NA MAJI KWA MIFUGO WATAJWA KUWA CHANZO CHA UTOVU WA USALAMA BONDE LA KERIO.

Mizozo mingi ambayo imekuwa ikishuhudiwa maeneo ya mipakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani za Elgeyo marakwet na Turkana na kupelekea hali ya utovu wa usalama inatokana na lishe pamoja na maji kwa ajili ya mifugo.

Mshirikishi wa mradi wa Kenya climate smart agriculture kaunti hiyo Philip Ting’aa alisema kwamba wengi wa wakazi wa maeneo hayo wanakosa lishe na maji kwa ajili ya mifugo wao hali inayowalazimu kuvuka katika kaunti nyingine na kuchangia mizozo hiyo.

Ting’aa alisema kwamba kama njia moja ya kuhakikisha mizozo hiyo inakabiliwa, mradi huo umechimba vidimbwi kadhaa vya kuhifadhi maji hasa maeneo hayo ya mipakani kuhakikisha kwamba wakulima wanapata maji kwa ajili ya mifugo yao na kuwazuia kwenda maeneo ya mipakani.

“Ukosefu wa maji na lishe ndicho chanzo kikuu cha utovu wa usalama katika mipaka ya kaunti hii na kaunti za Elgeyo marakwet na Turkana. Baadhi ya maswala ambayo tunafanya ni kuchimba vidimbwi vya maji kwa ajili ya mifugo ili kuzuia hali ambapo wafuhaji wanalazimika kuvuka mipaka na kusababisha mizozo na wakazi wa maeneo husika.” Alisema Ting’aa.

Aidha Ting’aa alisema kwamba mradi huo umetoa nyasi za kupanda kwa wakulima maeneo hayo kwa ajili ya mifugo wao, akitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima kujiunga katika mashirika ambayo yatafanya rahisi kusaidiwa katika maswala mbali mbali ya kilimo.

Tunawapa pia wafugaji nyasi aina mbali mbali na tunawaeleza kwamba watenge sehemu ya kupanda nyasi hizi kwa sababu wakitegemea tu nyasi hii ya kawaida haitatosha.” Alisema.