UHABA WA BARABARA NA MTANDAO WATAJWA KUWA KIZINGITI KATIKA JUHUDI ZA KUWAKABILI WAHALIFU BONDE LA KERIO.

Ukosefu wa barabara nzuri na tatizo la mtandao ni baadhi ya maswala ambayo yanafanya vigumu kukabili hali ya utovu wa usalama maeneo ya mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti zingine za bonde la kerio.

Akizungumza katika kikao na wadau mbali mbali katika mkahawa wa Horizon kuangazia mikakati ya jinsi ya kushughulikia usalama, waziri wa utumishi wa umma kaunti hiyo Martine Lotee alielezea haja ya kushughulikiwa changamoto hizo ili kutoa nafasi bora kwa maafisa wa usalama kuimarisha doria.

“Tunajaribu kufanya mikutano ya usalama kila mara ili kuimarisha hali ya usalama. Baadhi ya changamoto ambazo zipo maeneo hayo ni ukosefu wa barabara za kiusalama pamoja na mtandao ambapo mawasiliano ni tatizo.” Alisema Lotee.

Aidha Lotee alitaka kuanzishwa miradi mbadala maeneo hayo ili kuwapa wakazi nafasi ya kujishughulisha na maswala mengine kama vile kilimo na kutotegemea tu mifugo anayosema kwamba ndicho chanzo kikuu cha visa vya utovu wa usalama.

“Tungeomba pia serikali kuanzisha miradi mingine ambapo wakazi watajishughulisha nayo na kutotegemea tu mifugo, kwa sababu wahalifu wanaosababisha utovu wa usalama maeneo hayo wanalenga mifugo.” Alisema.

Wakati uo huo Lotee alitumia fursa hiyo kupongeza mikakati ambayo inaendelezwa na serikali maeneo hayo katika juhudi za kuhakikisha kwamba hali ya usalama inarejea, hasa mipango ya ujenzi wa kituo cha polisi eneo la lami nyeusi pamoja na shule kulingana na ahadi ya waziri wa usalama Kithure Kindiki.

“Ipo baadhi ya mikakati ambayo serikali inaweka kudhibiti hali ya usalama ikiwemo mipango ya kujenga kituo cha polisi eneo la lami nyeusi, pamoja na kujenga shule kuhakikisha watoto eneo hilo wanapata elimu. Kwa hivyo tunashukuru maana tunafahamu kwamba hatua hii itasaidia kukabiliana na utovu wa usalama.” Alisema.