UCHUNGUZI WAENDELEZWA KUHUSIANA NA KUPOTEA CHAKULA CHA MSAADA ENEO LA KANYARKWAT.
Baadhi ya viongozi eneo bunge la Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu kupotea kwa chakula cha msaada ambacho kilitolewa na serikali kwa ajili ya wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa eneo la Kanyarkwat.
Wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Riwo David Alukulem na mwenzake wa mnagei Richard Todosia viongozi hao walidai kwamba wakazi wa eneo hilo hawajakuwa wakipokea chakula hicho kuanzia mwezi januari mwaka huu licha ya kuwa kimekuwa kikitolewa na serikali.
Walisema kwamba wananuia kufanya kikao na wakuu wa usalama wakiongozwa na wasaidizi wa naibu kamishina eneo hilo ili kutoa mwanga zaidi kuhusiana na hali hiyo.
“Tumepata habari kwamba watu wa Kanyarkwat hawajakuwa wakipata chakula cha msaada ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali kuanzia mwezi januari mwaka huu. Kwa hivyo hatutakubali mambo kama haya. Tunaandaa kikao na wakuu wa usalama eneo hilo na kisha tutoe ripoti yetu ya mwisho kuhusiana na swala hili.” Walisema
Wakati uo huo viongozi hao waliwataka wakuu wa shule kuhakikisha kwamba chakula ambacho kinatolewa kwa shule na serikali kinatumika vyema wakionya dhidi ya mwalimu yeyote kuchukua chakula ambacho kinafaa kuwanufaisha wanafunzi.
“Hatujafurahia pia taarifa ambazo tunapata kutoka shule mbali mbali kwamba chakula kinachotolewa kwa ajili ya wanafunzi hakimalizi hata wiki moja. Kwa hivyo tunatoa onyo kwa wakuu wa shule kwamba yeyote atakayepatikana akichukua chakula kinachonuiwa kuwasaidia wanafunzi atakabiliwa kisheria.” Walisema.