UCHUNGUZI WAANZISHWA KUHUSU KUTEKETEA BWENI LA SHULE YA ST. BRIDGIT’S KIMININI.
Kamishina wa kaunti ya Trans nzoia sam Ojwanga ameahidi kuimarisha usalama katika shule hasa za mabweni ili kukabili visa vya majengo kuteketea shuleni.
Akizungumza muda mfupi tu baada ya bweni la orofa mbili kuteketea katika shule ya upili ya kitaifa ya wasichana ya St Bridgits Kminini, Ojwanga amesema kuwa wameanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo akisisitiza kuwa iwapo mtu atapatikana kuhusika na kisa hicho atachukuliwa hatua kali.
Moto huo ulianza takriban saa moja usiku wa kuamkia leo wakati wanafunzi wakiwa darasani huku ikikisiwa awali kuwa huenda ulisababishwa na hitilafu katika mfumo wa umeme.
Ni kisa kinachojiri chini ya mwezi mmoja tu baada ya shughuli za masomo kurejelewa kwa muhula wa kwanza huku wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wakiendelea kuripoti shuleni kwa wiki ya pili sasa.