Uchimbaji haramu wa madini wazidi kuibua tumbojoto pokot magharibi

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi John Lonyangapuo, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia uchimbaji madini haramu ambao unaendelezwa na watu fulani.


Wakizungumza eneo la Sigor, viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo John Lonyangapuo na mbunge wa Kapengiria Samwel Moroto miongoni mwa viongoizi wengine, walisema shughuli ya uchimbaji madini imeharibu mazingira.

“Nimetembea maneo ambako kunachimbwa madini na kushuhudia hali ilivyo, ni ya kusikitisha. Shughuli hii ambayo inaendeshwa kwa njia haramu imeharibu sana mazingira yetu na huenda tukawa katika hali ya hatari,” alisema Lonyangapuo.


Viongozi hao walidai huenda wanaoendeleza uchimbaji madini kaunti hiyo kinyume cha sheria wanalindwa na watu wenye mamlaka serikalini, kwani tangu lalama kuhusiana na shughuli hii zianze kutolewa, idara husika imesalia kimya.


“Wale ambao wanawalinda wanaoendeleza uchimbaji haramu lazima wajitokeze. Tumelalamika kwa muda kuhusiana na shughuli hii lakini wahusika wamesalia kimya,” alisema Moroto.


Hata hivyo akijibu madai hayo, kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Abdulahi Khalif alisema kwamba hana haja na kujihusisha na shughuli yoyote ya uchimbaji madini, ila jukumu lake ni kuhakikisha wakazi wa kaunti hiyo wanapokea huduma bora.


“Nimeambiwa mara nyingi kwamba najihusisha na uchimbaji madini kaunti hii. Mimi sina haja na madini. Kazi yangu hapa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanahudumiwa vyema,” alisema Khalif.


Wakati uo huo Khalif alisema kwamba raia saba wa uchina ambao walikamatwa wakiendeleza shughuli ya uchimbaji madini haramu walichukuliwa hatua huku baadhi yao wakirudishwa nchini mwao kwa kuwa nchini kinyume cha sheria.


“Wale ambao walikuwa wanajihusisha na shughuli ya uchimbaji madini kinyume cha sheria walichukuliwa hatua. Raia saba wa Uchina walikamatwa na hata wawili wakarejeshwa nchini kwao kwa kuwa nchini kinyume cha sheria,” alisema.