UBALOZI WA UHOLANZI WAIMARISHA MIKAKATI YA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.
Balozi wa uholanzi nchini Maarten Brouwer amefanya kikao na gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin kuangazia jinsi ambavyo serikali ya kaunti hiyo itashirikiana na taifa hilo katika maswala mbali mbali na jinsi ya kuimarisha mikakati ya kuhakikisha maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kikao na balozi huyo afisini mwake, gavana Simon Kachapin alisema kwamba wamegusia maeneo mengi ya ushirikiano baina ya kaunti hiyo na taifa la uholanzi ikiwemo maswala ya ugatuzi, ugaidi miongoni mwa maswala mengine.
Kachapin amelipongeza taifa hilo kwa uhusiano mwema ambao limekuwa nao na kaunti ya Pokot magharibi kwa muda sasa na ambao umepelekea kuimarishwa sekta mbali mbali kwa manufaa ya wakazi hasa ya afya, Kacheliba na sigor zikinufaika pakubwa.
“Tumekubaliana kushirikiana katika sehemu nyingi ikiwemo kukabili maswala ya ugaidi, miradi ya kukabiliana na hali ya ukame, maswala ya ugatuzi miongoni mwa maswala mengi ambayo tumeyajadili na Balozi Brouser.” Alisema Kachapin.
Kwa upande wake balozi Brouwer alisema kwamba taifa hilo la Uholanzi limekuwa mshirika mkuu wa taifa la Kenya hasa kuhusiana na maswala ya kibiashara na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha alisema taifa hilo limeelekeza ushirikiano huo hadi kwenye serikali za kaunti kupitia kuhakikisha fedha zinakuwepo kufanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
“Uholanzi imekuwa mshirika mkuu wa Kenya katika maswala ya kibiashara pamoja na kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kwa sasa tumeamua kupanua ushirikiano wetu na Kenya ambapo sasa tunatembelea kaunti mbali mbali kuhakikisha kwamba tunafanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo.” Alisema Brouser.