‘TUPO TAYARI KUKABILI CORONA’ SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI.


Licha ya kulaumiwa kwa kutojiandaa kukabili janga la corona, serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi imesema kuwa imejiandaa kikamilifu kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo iwapo vitaripotiwa kuongezeka kaunti hii.
Waziri wa afya kaunti hii ya Pokot magharibi Christine Apakoreng amesema kuwa vipo vitanda vya kutosha kuwashughulikia wagonjwa ambao watahitajika kulazwa katika hospitali mbali mbali ikiwemo ya Kapenguria, akiongeza kuwa kituo kingine kimefunguliwa eneo la Aramaket ambacho kina vitanda 20.
Aidha Apakoreng amesema kuwa madaktari zaidi 35 wameajiriwa kuimarisha sekta ya afya huku akiongeza kuwa serikali ya kaunti ililazimika kuwaita tena wahudumu wa afya ambao mkataba wao wa kuhudumu kwa mwaka mmoja ulikuwa imekamilika ili kupiga jeki juhudi za kuwahudumia wakazi.
Wakati uo huo Apakoreng amesema tangu kuripotiwa kisa cha kwanza cha virusi vya corona katika kaunti hii ya pokot magharibi mwaka jana, ni jumla ya watu 290 ambao walithibitishwa kuambukizwa kufikia sasa, huku akitoa wito kwa wakazi kuendelea kujitokeza ili kupewa chanjo dhidi ya virusi hivyo.