Tunapasa kubadilisha dhana ya kutegemea ufugaji kupitia elimu; Mastaluk

Richard Mastaluk Mwakilishi wadi ya Kapenguria, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuwahimiza wazazi kukumbatia elimu ya wanao kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye.


Mwakilishi wadi ya Kapenguria Richard Mastaluk ambaye alizungumza jumanne katika hafla moja eneo la Kacheliba alisema ni wakati wakazi wanapasa kukumbatia elimu ili kaunti hiyo iweze kuafikia viwango vya kaunti zingine nchini.


Aidha Mastaluk alisema tamaduni ya kutegemea ufugaji wa ng’ombe kuwa kitega uchumi kikuu katika kaunti hiyo inapasa kukoma, na wakazi kujihusisha na shughuli zingine za kuwapa kipato kutokana na elimu ambayo wamepokea.


“Ili tubadilishe hii desturi kwamba ufugaji wa ng’ombe ndiyo shughuli yetu pekee ya kujipatia mapato, ni lazima tuwapeleke watoto wetu shule wapate maarifa ya kujishughulisha na kazi zingine zitakazoimarisha jamii zetu,” alisema Bw. Mastaluk.


Wakati uo huo Bw. Mastaluk aliwahimiza wazazi kujitenga na tamaduni ya ukeketaji na kuwapa fursa wanao wa kike kusoma ili kuafikia ndoto zao, akiwataka wakazi wa kiume kuchangia katika juhudi za kukomesha tamaduni hiyo.


“Nataka kuwahimiza vijana wetu kwamba wana nafasi ya kuhakikisha utamaduni wa ukeketaji unakomeshwa katika jamii yetu. Wanapasa kutambua kwamba mwanamke mzuri ni yule ambaye hajakeketwa,” alisema.