Tukome kuzungumzia mabaya ya serikali, tuangazie mema; Lotee

Titus Lotee Mbunge wa Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi, Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Wandani wa rais William Ruto katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kumtetea kutokana na utendakazi wake tangu alipoingia mamlakani.


Wakiongozwa na mbunge wa Kacheliba Titus Lotee, viongozi hao walisema serikali ya Kenya kwanza imefanya juhudi zote kuhakikisha maslahi ya wananchi yanafanywa kipau mbele japo wananchi wengi wameonyesha kutoridhishwa na juhudi hizo.


Lotee alisema kwamba inasikitisha kuona kwamba wakenya wanaangazia zaidi mabaya yanayodaiwa kutekelezwa na serikali ya Kenya kwanza huku wakiyafumbia macho mengi mema ambayo inatekeleza kwa manufaa ya wananchi.


Alitolea mfano miradi mbali mbali hasa ya maji ambayo serikali ya rais William Ruto imetekeleza katika kaunti hiyo, akisema hii ni ishara tosha kwamba serikali yake ina malengo mazuri katika kuimarisha maisha ya wakenya.


“Nashukuru serikali kwa kazi inayofanya. Na nafikiria ni wakati ambapo kama wakenya tunapasa kutambua kile ambacho serikali inafanya. Mara nyingi tunazungumza mabaya kuhusiana na serikali bila kuona mema ambayo inatekeleza,” alisema Bw. Lotee.


Lotee aliwataka wananchi kutoikosoa serikali kila mara na badala yake kuangazia pia mema ambayo imetekeleza katika kipindi ambacho imekuwa uongozini, na iwapo hawajaridhishwa na utendakazi wake basi wafanye maamuzi ya busara katika uchaguzi mkuu ujao.


“Ni muhimu kwa wakenya kutambua kwamba serikali hii inabadilisha mazingira. Watu ambao wamenufaika na miradi ya serikali wanapasa kukoma kuizungumzia mabaya na badala yake kufurahia matunda ya serikali hii,” alisema.