TSC YATANGAZA KUANZA SHUGHULI YA KUWAAJIRI WALIMU ZAIDI POKOT MAGHARIBI WAKAZI WAKIONYWA DHIDI YA MATAPELI.
Tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti ya Pokot magharibi imesema kwamba inanuia kuwaajiri walimu zaidi ili kushughulikia changamoto ya uhaba wa walimu katika shule za kaunti hiyo pamoja na kuhakikisha kuna walimu wa kutosha kufanikisha mtaala mpya wa elimu CBC.
Mkurugenzi wa tume hiyo Bernad Kimachas alisema kwamba jumla ya walimu 107 wataajiriwa katika shule za msingi, 22 kati yao wakiwa wa mkataba wa kudumu huku 85 wakihudumu katika mafunzo ya nyanjani, walimu 629 wakiajiriwa katika shule za upili, 105 wakihudumu katika mkataba wa kudumu huku 444 wakihudumu katika masomo ya nyanjani.
“Tunalenga kuwaajiri jumla ya walimu 107 wa shule za msingi, 22 miongoni mwao wakiajiriwa kwa mkataba wa kudumu huku 85 wakihudumu kwa masomo ya nyanjani. Katika shule za upili tutawaajiri walimu 629, walimu 185 miongoni mwao kwa mkataba wa kudumu huku 444 wakihudumu katika masomo ya nyanjani.” Alisema Kimachas.
Kimachas aidha alisema kwamba watu wanaoishi na changamoto za ulemavu watapewa kipau mbele katika zoezi hilo la usajili wakihudumiwa kwa njia spesheli, huku akitumia fursa hiyo kuwahimiza kutuma maombi ya kusajiliwa.
“Tutaweka sana makini yetu kwa watu wanaoishi na ulemavu. Kulingana na katiba tunahitajika kuajiri asilimia 5 ya watu hao na hawa tutawahudumia kwa njia spesheli.” Alisema.
Wakati uo huo Mkurugenzi huyo wa TSC aliwaonya wote wanaolenga nyadhifa hizo dhidi ya matapeli ambao huenda wakawahadaa kuwa watawasaidia kupata nyadhifa hizo, akisema kwamba zoezi la usajili wa walimu litakuwa wazi, na watakaofuzu pekee ndio watakaosajiliwa.
“Tunafahamu kwamba kuna matapeli ambao wanawahadaa watu kwamba wanaweza kuwasaidia kupata ajira. Tume ya TSC inapeana ajira bila kuuliza hongo wala kuhitaji ushawishi wowote. Nawahimiza wote kutohadaiwa kwani tunazingatia sheria katika kutoa ajira.” Alisema Kimachas.