TSC YATAKIWA KUTOA KIPAU MBELE KWA WAKAZI KATIKA SHUGHULI YA USAJILI WA WALIMU POKOT MAGHARIBI.


Wakazi wa eneo la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi hasa wanaotafuta nafasi za ajira katika zoezi linaloendelea la kuwaajiri walimu nchini wamelalamikia idadi kubwa ya watu wanaofika eneo hilo kutafuta nafasi hizo kutoka maeneo mengine ya nchi.
Wakiongozwa na Benard Lolem, wakazi hao walidai kwamba watu kutoka kaunti zingine ikiwemo Bungoma na Elgeyo marakwet wanafika eneo hilo kusaka nafasi za ajira wakitaka maafisa wanaoendeleza shughuli ya usajili kuhakikisha kwamba nafasi hizo zinawaendea wakazi kabla ya kuwajiri watu kutoka nje.
“Watu kutoka kaunti zingine ikiwemo Bungoma, Elgeyo Marakwet na hata Uasin Gishu wamekuwa wakija katika shughuli hii kusajiliwa. Kile tunasema ni kwamba tume ya TSC ihakikishe kwamba wakazi wa hapa wanapewa nafasi kwanza na zile zitabaki ndio wapee watu wa nje.” Alisema Lolem.
Ni hali ambayo ilishutumiwa vikali na mbunge wa eneo hilo Titus Lotee ambaye alisema kwamba kwa muda mrefu wakazi wa eneo hilo wamenyimwa nafasi za ajira huku watu kutoka maeneo mengine wakipewa nafasi hizo akisema kwamba kamwe hawatakubali hali hiyo kutokea katika zoezi hili.
“Watu walifanya maandamano wakilalamika kwamba kuna watu ambao wametoka nje wengi wakitaka kuchukua nafasi za watu wa Kacheliba. Nasema kwamba hilo si jambo zuri. Sisi kama watu wa Kacheliba tumefinywa sana kwa miaka mingi kwa sababu watu wanatoka nje na kupewa kazi huku watoto wetu wakiendelea kuumia. Kwa hivyo tunasema wakati huu hatutakubali hilo.” Alisema Lotee.
Naibu kamishina wa Kacheliba Kanneth Kiprop aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa swala hilo litashughulikiwa akiwataka wote wanaotafuta nafasi hizo kuwa watulivu maafisa wa TSC wanapohakikisha kwamba zoezi hilo linaendeshwa kwa haki.
“Yale maswala ambayo yameibuliwa hapa yatashughulikiwa. Kile ninachowahimiza wote waliofika hapa ni kuwa watulie kwa sababu TSC itawatendea haki. Tutahakikisha kwamba zoezi hili linaendeshwa kwa haki ili kila mtu aridhike.” Alisema Kiprop.