TSC YASHUTUMU VISA VYA UVAMIZI DHIDI YA WALIMU POKOT MAGHARIBI.
Tume ya huduma kwa walimu TSC imeshutumu vikali visa vya uvamizi dhidi ya walimu katika kaunti ya Pokot magharibi ambavyo vimeripotiwa kukithiri.
Akirejelea kisa cha hivi majuzi cha kuvamiwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Sabina eneo la Sook, mkurugenzi wa tume hiyo kaunti ya Pokot magharibi Benard Kimachas alisema ni jambo la kusikitisha kwa wanafunzi au jamii kuwavamia walimu ambao ndio wanaokusudiwa kutoa huduma za kuielimisha jamii.
Kimachas alitoa wito kwa jamii kuwasilisha malalamishi kwa afisi yake iwapo hawajaridhika na utendakazi wa mwalimu husika badala ya kuwavamia na kuwasababishia majeraha.
“Inasikitisha sana kuona kwamba walimu ambao tunategemea kuipa elimu jamii sasa wanafanya kazi kwa kuhofia usalama wao mikononi mwa jamii ambayo wanapasa kuihudumia. Jamii inapasa kufahamu kwamba kazi ya mwalimu ni kufunza, na iwapo kuna malalamishi dhidi ya mwalimu husika, ni vema kuyawasilisha kwa idara husika badala ya kuwavamia.” Alisema Kimachas.
Alisema kwamba tume hiyo huwatuma walimu katika shule mbali mbali kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii na iwapo sasa itafika kiwango cha maisha yao kuwa hatarini basi huenda wakalazimika kuwaondoa walimu hao hali ambayo itaathiri viwango vya elimu kaunti hiyo.
“Sisi kama tume tunawatuma walimu kutoa huduma kwa jamii, na iwapo sasa imefikia kiwango ambapo maisha ya walimu wetu yamo hatarini, itatulazimu basi kuwaondoa ili maeneo haya yasalie bila walimu.” Alisema.