TSC YAKIRI KUWEPO UPUNGUFU MKUBWA WA WALIMU KATIKA SHULE ZA MASHINANI POKOT MAGHARIBI.

Shule za maeneo ya mashinani kaunti ya Pokot magharibi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu kutokana na hatua ya serikali kusitisha utekelezwaji wa sera ya kuwataka walimu kufunza mbali na kaunti zao za nyumbani ambapo wengi wa walimu wamerejea katika kaunti zao.

Kaimu mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti ya Pokot magharibi Jane Nyakoe amesema kwamba walimu wengi wameondoka katika shule hizo na wanaorejea kaunti hiyo hawataki kuelekea kufunza katika shule hizo za mashinani.

Nyakoe alitoa wito kwa viongozi kaunti hiyo kushirikiana na tume hiyo katika kuhakikisha kwamba shule hizo zinapata walimu ili pia wanafunzi maeneo hayo waweze kuhudumiwa kama wanafunzi wa maeneo mengine nchini.

“Walimu wengi wameamua kwenda katika kaunti zao za nyumbani baada ya serikali kusitisha sera ya kuwapa uhamisho walimu hadi kaunti za mbali na kwao. Hali hii imeathiri pakubwa shule za maeneo ya mashinani kwa kuwa wengi wao walikuwa wakifunza katika shule hizo.” Alisema Nyakoe.

Wakati uo huo Nyakoe alisema kaunti hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu zaidi ya alfu 1,800 katika shule za msingi, alfu moja katika shule za sekondari ya msingi huku shule za upili zikikabiliwa na upungufu wa takriban walimu 800, akitoa hakikisho la wakazi wa kaunti hiyo kupewa kipau mbele katika usajili mpya wa walimu hao.

“Tuna upungufu wa walimu zaidi ya 1,800 katika shule za msingi, 100 katika shule za sekondari ya msingi na 800 katika shule za upili. Katika zoezi hili la usajili wa walimu tunahakikisha kwamba kipau mbele kinapewa wakazi wa kaunti hii.” Alisema.