TSC yaahidi kushughulikia uhaba wa walimu Pokot magharibi

Gavana wa kaunti ya pokot magharibi Simon Kachapin akikagua jengo la shule ya Siyoi, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba tatizo la upungufu wa walimu ambao unashuhudiwa litashughulikiwa hivi karibuni na tume ya huduma kwa walimu TSC.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miundo mbinu inayojengwa kwa ufadhili wa wakfu wa Safaricom kwenye shule ya msingi ya Siyoi, gavana Kachapin alisema alifanya kikao na mwenyekiti wa tume ya TSC ambaye alimhakikishia kwamba tatizo hilo litaangaziwa.
Gavana Kachapin alisisitiza kwamba kaunti hiyo inapasa kupewa kipau mbele kwenye swala la uajiri wa walimu kutokana na hali kwamba ilisalia nyuma kwa miaka mingi, akiahidi kufuatilia kuhakikisha swala hili linatimizwa, ili kaunti hiyo pia iweze kufikia viwango vya kaunti zingine kimaendeleo.
“Tulikutana juzi na mwenyekiti wa tume ya kuajiri walimu TSC tukazungumzia maswala ya walimu kwa mapana, akasema kwamba sehemu kama Pokot magharibi ambayo ilisalia nyuma, atafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba upungufu wa walimu unashughulikiwa,” alisema Bw. Kachapin.
Gavana Kachapin aliupongeza wakfu huo wa Safaricom kwa ujenzi wa miundo mbinu katika shule hiyo ya Siyoi na shule zingine kadhaa kaunti hiyo ambayo alisema itafaa sana hasa katika mfumo mpya wa elimu wa CBE akiahidi ushirikiano mkamilifu wa serikali yake kuhakikisha malengo yanaafikiwa.
“Kila jengo ambalo lipo hapa limekusudia kiwango ambacho kinapasa kuwa katika shule ya msingi hasa kwenye mfumo huu wa elimu wa CBE. Kwa hivyo mimi kama gavana nafurahi kwa sababu shule hii itakuwa moja ya shule ambazo zimejengwa vizuri katika kaunti yetu,” alisema.