TODOSIA AAPA KUAFIKIA MATAKWA YA WANANCHI PUNDE BAADA YA KUAPISHWA.


Mwakilishi wadi mteule wa mnagei katika kaunti hii ya Pokot magharibi Richard Todosia amewapongeza wakenya kuwa kuendelea kudumisha amani kipindi chote cha uchaguzi hadi pale mahakama ya juu ilipodumisha ushindi wa rais mteule William Ruto.
Akizungumza baada ya kuandaa ziara za maeneo mbali mbali ya wadi ya mnagei kukagua sehemu ambazo zinastahili kuangaziwa katika uongozi wake wa wadi hii, Todosia amesema kuwa taifa litaafikia mengi chini ya rais mteule William Ruto pindi atakapoapishwa.
Todosia amesisitiza kwamba Ruto alichaguliwa kwa njia ya halali kulingana na katiba ya taifa na kupuuzilia mbali wapinzani wake wa kisiasa ambao walielezea kutoridhishwa na uamuzi wa mahakama ya juu uliodumisha ushindi huo.
“Mahakama ya juu ilithibitisha kuwa Ruto alichaguliwa kwa njia ya halali na kikatiba. Hivyo natumia tu fursa hii kuwashukuru wakenya kwa kuzingatia amani na nina imani kwamba Ruto ndiye chaguo bora la kusuluhisha matatizo ya taifa hili.” Alisema.
Wakati uo huo Todosia amewataka wakazi kutokuwa na hofu akiahidi kwamba atashirikiana na wadau kutoka sekta mbali mbali kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili wakazi wa mnagei zinashughulikiwa ipasavyo pindi atakapoapishwa rasmi kuanza majukumu yake.
“Nimetembelea maeneo mbali mbali ya wadi hii ya Mnagei na nimeorodhesha maswala ambayo nitayashughulikia punde tu baada ya kuapishwa. Nitatafuta wadau wa eneo hili ili tuone jinsi tutashughulikia maswala hayo.” Alisema.