TODOSIA AAHIDI KUTOA KIPAU MBELE KWA SWALA LA ELIMU MNAGEI.

Mwakilishi wadi ya Mnagei eneo bunge la Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Richard Todosia ameahidi kutoa kipau mbele kwa miundo mbinu ya sekta ya elimu ili kuimarisha viwango vya elimu eneo hili.

Todosia amesema kwamba atazungumza na serikali pamoja na wadau wengine katika juhudi za kuhakikisha kwamba madarasa ambayo yalikuwa yakijengwa katika shule za wadi hii yanakamilishwa kando na kuhakikisha zinapata viwanja kwa shule ambazo hazina.

Aidha Todosia amesema atahakikisha miundo msingi yote inayohitajika kufanikisha elimu inajengwa katika utawala wake.

Tutazungumza na wadau kama serikali ya kitaifa na wahisani wengine kuhakikisha kwamba madarasa yaliosalia yanakamilishwa katika shule za wadi hii. Shule ambazo hazina viwanja pia tutahakikisha kwamba zinashughulikiwa.” Alisema.

Aliongeza kwamba, “ Kuna shule ambazo hazina miundo msingi hitajika katika wadi hii na katika utawala wangu nitahakikisha kwamba kila shule ina miundo msingi mizuri na hitajika kwa masomo ya wanafunzi.”

Todosia amesema kwamba lengo lake ni kuhakikisha ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo hamna mwanafunzi kutoka wadi ya Mnagei anayelazimika kutembea kwa mwendo mrefu kupata elimu wala wanafunzi kusomea chini ya miti kwa ukosefu wa madarasa.

“Ninawahakikishia watu wa Mnagei kwamba nitazungumza na viongozi wetu wa kaunti na wale wa kitaifa kuhakikisha kwamba ndani ya miaka mitano hakuna mwanafunzi ambaye atatembea mwendo mrefu kutafuta elimu wala anayesomea chini ya mti.” Alisema Todosia.

[wp_radio_player]