Tamaduni zilizopitwa na wakati zatajwa kuwa changamoto kwa maendeleo ya mtoto wa kike

Na Benson Aswani,
Mtoto wa kike katika kaunti ya Pokot magharibi ana uwezo wa kuafikia upeo wa juu zaidi iwapo atapewa nafasi na njia ya kuafikia upeo huo.
Akizungumza katika hafla ya kuwapa ushauri watoto wa kike eneo la Murpus, mkurugenzi wa shirika la Circle group Limited Asmahan Pogal aliitaka jamii kujitenga na tamaduni ambazo zimekuwa zikimrudisha mtoto wa kike nyuma na kumpa nafasi ya kudhihirisha uwezo wake kielimu na kitaaluma.
“Watoto wa kike katika kaunti hii wana uwezo wa kuafikia upeo wa juu zaidi iwapo tu watapewa nafasi hiyo. Ni jukumu letu kama jamii kuhakikisha kwamba tunawapa muda wa kuafikia ndoto zao kwa kuwaepusha na tamaduni zilizopitwa na wakati,” alisema Bi. Pogal.
Kauli yake ilisisitizwa na mkurugenzi wa shirika la Perur Rays of Hope Carolyne Menach ambaye aidha aliwataka watoto wa kike kujipa ujuzi mbali mbali si darasani pekee bali pia shughuli mbali mbali katika jamii.
“Tukiweza kuwapatia fursa ya kujijenga, fursa ya kutengeneza nchi iwe bora, hao watoto pia watakuwa na maisha bora. Kwa hivyo tunawahimiza watilie mkazo masomo yao, na pia kujipatia ujuzi tofauti si kupitia darasa tu bali pia shughuli tofauti katika jamii,” alisema Bi. Menach.
Kwa upande wake naibu kamishina eneo la Kipkomo Sheila Imbaga aliwataka wazazi kukumbatia elimu ya mtoto wa kike akielezea wasiwasi wa idadi ya chini ya watoto hao katika shule za msingi.
“ Zipo baadhi ya tamaduni ambazo zinamfanya mtoto wa kike kupotea. Tukiangalia idadi ya watoto wasichana imeendelea kupungua sana,” alisema Bi. Imbaga.
