TAMADUNI ZATAJWA KUWA KICHOCHEO CHA MIMBA ZA MAPEMA MIONGONI MWA WATOTO POKOT MAGHARIBI.

Mimba za mapema miongoni mwa watoto katika kaunti  ya Pokot magharibi zinachangiwa na hali kwamba jamii haijakumbatia swala la kuzungumzia wazi maswala ya ngono kwa watoto kutokana na hali inayotajwa kuchangiwa na tamaduni mbali mbali.

Haya ni kulingana na afisa anayesimamia idara ya watoto kaunti hiyo Philip Opopa ambaye alisema hali hii imefanya watoto kutolindwa dhidi ya mahusiano ya kiholela, japo akikiri kushirikiana na wadau mbali mbali kubuni mikikakati ya kushughulikia hali hiyo kwa njia mbadala.

“Jamii haiwezi kuzungumzia wazi kuhusu maswala ya ngono na watoto kwa sababu wanaamini kwamba ni kinyume cha tamaduni za kiafrika na hili linafanya watoto kutolindwa dhidi ya mahusiano ya kiholela. Tunashirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha usalama wa watoto kupitia njia mbadala.” Alisema Opopa.

Wakati uo huo Opopa alisema kwamba wanaendeleza mikakati ya kuhakikisha idara ya watoto imetengewa bajeti yake ya kutosha ili kushughulikia maswala ambayo yamekuwa yakiwakumba watoto katika jamii bila changamoto zozote.

“Ipo mikakati ambayo itawezesha serikali kutenga bajeti kwa ajili ya idara ya watoto ambayo itasaidia katika kushughulikia maswala ambayo yanawaathiri watoto.” Alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa mradi wa accelerate John Chege alisema mashirika mbali mbali yanashirikiana kubuni sheria za kuwalinda watoto dhidi ya dhuluma za jinsia kama vile ndoa za mapema pamoja na ukeketaji.

“Mara nyingi watoto hawapo salama kuhusiana na dhuluma za jinsia. Kama wadau tunaendeleza mikakati ya kubuni sheria ambazo zitawalinda watoto dhidi ya ukeketaji na ndoa za mapema katika viwango vya kaunti.” Alisema Chege.