TAHARUKI YAENDELEA KUTANDA OMBOLION MTU MMOJA AKIULIWA NA WAVAMIZI.


Hali ya taharuki imetanda katika eneo la ombolion, turkwel mpakani mwa kaunti za pokot magharibi na turkana baada ya kijana wa miaka 18 kuuliwa na wavamizi wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani kwa nia ya kuiba mifugo.

Uvamizi huo wa mwendo wa saa saba jana ulisababisha kifo cha kijana huyo aliyeamua kukabiliana nao.

Naibu chifu wa eneo hilo joseph korkimul amethibitisha tukio hilo akisema kuwa maafisa wa polisi wanaendelea kuwasaka washukiwa.

Aidha amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu wakati huu wa uchaguzi na kuonya kuwa serikali inaendelea kuimarisha usalama eneo hilo la mpakani.

Ni kisa kinachojiri siku chache tu baada ya watu saba kuteketea hadi kufa baada ya wavamizi kuvamia kijiji cha Napeitom kaunti ya Turkana huku pia wakiteketeza nyumba kadhaa.

Makundi ya wanawake katika kaunti hiyo yaliandaa maandamano hadi katika afisi ya kamishina wa kaunti ya Turkana Wambua Muthama wakilalamikia utovu wa usalama ambao umekithiri maeneo hayo.

Wanawake hao ambao waliongozwa na Cecilia Ishur walimtaka waziri wa usalama wa ndani ya nchi Dkt. Fred Matiangi kufika Turkana na kuwaeleza kuhusu hatua ambazo zimepigwa kukabili utovu huo wa usalama.

“Your Excellency president Uhuru Kenyatta, the same same kapedo hapo ndio askari wako waliuawa siku ile ukalia kwa uchungu. Hii ya wamama wamechomwa kama mbuzi nyinyi bado hamjaongea, hakuna ndege ya serikali imeland hapo kwa scene of crime mpaka saa hizi mnangoja nini? Sisi tunasema kama hakuna serikali kutushughulikia tutajishughulikia wenyewe.” Alisema Ishur.

Waandamani hao walisema kuwa eneo bunge la Turkana mashariki hasa wadi ya Kapedo Napeitom imeathirika pakubwa.

Mbunge wa Turkana ya kati John Lodepe aliilaumu wizara ya usalama wa ndani kwa kukosa kuwajibika.

“Sisi tunataka Matiangi mwenyewe akuje. Kwa sababu mtu akipigwa hapo Nairobi Matiangi anakimbia, mwizi akiuliwa, Matiangi anakimbia, Kibicho anakimbia, serikali inakimbia, lakini mturkana akiuliwa pamoja na mali yake hakuna mtu anakuja. Kumaanisha kwamba maisha ya waturkana hayana faida.” Alisema Lodepe.

Siku ya jumatatu mratibu wa bonde la ufa Maalim Mohammed alisema kuwa maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa eneo la Napeitom kusaka wahalifu hao na wote waliotekeleza uovu watafikishwa mahakamani.