SWALA LA USALAMA LASALIA KIZUNGUMKUTI BONDE LA KERIO VIONGOZI WAKIZIDISHA HARAKATI ZA KUAFIKIWA AMANI.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wanaendeleza juhudi mbali mbali za kuhakikisha kwamba visa vya uvamizi ambao unaendelea kushuhudiwa maeneo ya mipakani vinakabiliwa ili kuafikia amani na kuruhusu wakazi wa maeneo hayo kuendeleza shughuli zao za kawaida.

Mwakilishi wadi ya Lomut Jacob Tong’ole alisema kwamba kundi la waakilishi wadi kutoka kaunti hiyo hasa wadi zinazoshuhudia tatizo la usalama kwa ushirikiano na wenzao kadhaa kutoka kaunti jirani ya Elgeyo marakwet wameanzisha harakati za kuhakikisha amani inadumishwa maeneo hayo.

Tong’ole alisema kwamba ni wakati ambapo wananchi wa maeneo hayo wanapasa kutumia raslimali zinazopatikana eneo hilo ambazo hawajazitumia kwa muda kufuatia tatizo la usalama, akitoa wito kwa viongozi wengine kuwaunga mkono katika safari hiyo kuhakikisha kwamba juhudi zao zinafanikiwa.

“Tumeanzisha harakati waakilishi wadi kadhaa kaunti hii kwa ushirikiano na wenzetu kutoka Elgeyo marakwet za kuhakikisha kwamba amani inadumishwa. Kwa sababu tunataka watu wetu watumie raslimali zilizopo. Kile tunaomba tu ni uungwaji mkono kutoka viongozi wetu wa juu.” Alisema Tongole.

Wakati uo huo Tong’ole alivitaka vitengo vya usalama pia kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa wananchi na mali yao inavyopasa, na hata kuwataja kwa majina wahalifu wanaoendeleza uhalifu maeneo hayo ili kuwapa wakazi nafasi ya kutekeleza shughuli zao kwa amani.

“Nawaambia maafisa wa usalama wa vitengo vyote kuhakikisha kwamba maisha ya wakazi na mali yao inalindwa, na hata ikiwezekana wawataje wahalifu hao kwa majina ili watu wetu wapate wakati wa kutekeleza shughuli zao kwa amani.” Alisema.