SPIKA MUKENYANG KUHUDHURIA KIKAO CHA KWANZA TANGU KUBANDULIWA POKOT MAGHARIBI.


Kivumbi kinatarajiwa katika bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi linaporejelea vikao vyake hii leo baada ya mapumziko ya mwezi mmoja.
Spika wa bunge hilo Catherine Mukenyang anatarajiwa kuongoza vikao vya leo kwa mara ya kwanza tangu jaribio la kumbandua afisini ambalo hata hivyo lilisitishwa kwa muda na mahakama ya Eldoret ili kusikiliza kesi aliyowasilisha mukenyang kupinga kubanduliwa kwake.
Mukenyang alilalamikia kutopewa muda wa kujitetea na bunge hilo akidai kuwa baadhi ya wabunge katika bunge hilo walihongwa ili kuhakikisha kuwa anabanduliwa.
Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo ataongoza vikao hivyo vya leo ikizingatiwa zaidi ya wabunge 25 katika bunge hilo wameshikilia msimamo kuwa Mukenyang hafai kuhudumu kama spika licha ya kuwa na agizo la mahakama linalomkubalia kuendelea kuhudumu katika wadhifa huo.
Ikumbukwe Mukenyang aling’atuliwa mapema mwezi septemba kupitia hoja ya kutokuwa na imani naye iliyowasilishwa na mwakilishi wadi ya Endough Evanson Lomaduny kwa madai ya matumizi mabaya ya afisi, kukiuka sheria za bunge hilo na utovu wa heshima.