SIASA ZATAJWA KUCHANGIA KUTUPILIWA MBALI BBI.

Na Benson Aswani
Viongozi wa shirika la kidini la Women of faith kaunti hii ya Pokot magharibi wametaja siasa kuwa chanzo cha kutajwa mchakato wa kufanyia katiba marekebisho kupitia mpango wa upatanishi BBI kuwa kinyume cha sheria.
Wakizungumza baada ya kikao mjini Kapenguria viongozi hao wamesema kuwa licha ya mwafaka baina ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kuleta amani nchini na kuanzishwa mchakato wa BBI, siasa ziliingizwa katika mchakato huo na kupelekea mahakama kuutupilia mbali.
Hata hivyo viongozi hao wamedokeza kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea ili kuhakikisha baadhi ya maswala yaliyokuwa katika mswada huo yanatekelezwa kwa lengo la kuhakikisha amani inadumishwa nchini.
Wakati uo huo wametoa wito kwa wanasiasa kuendesha siasa zao kwa njia ya amani taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao na kutojenga mazingira ambayo huenda yakapelekea kushuhudiwa vurugu nchini jinsi ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.