SHULE ZASALIA MAHAME KACHELIBA KUFUATIA MAKALI YA NJAA

Shule nyingi eneo la Kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magaribi zinakosa mgao wa kutosha unaotolewa na serikali kuu kuendesha shughuli shuleni humo kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi katika shule hizo.

Akizungumza baada ya kikao na wadau wa elimu ikiwemo wakuu wa shule machifu na manaibu wao kupanga mikakati ya kuwapeleka watoto walio nyumbani shuleni, mkurugenzi wa elimu eneo la Kacheliba Edward Wangamati alisema kwamba utafiti uliofanywa unaonyesha kwamba idadi kubwa ya watoto eneo hilo hawahudhurii masomo.

“Utafiti wetu unaonyesha kwamba watoto wengi sana wako nje ya shule, na tumezungumza na walimu wakuu, machifu na manaibu wao kuhusu mikakati ya kuhakikisha kwamba watoto hao wanafika shuleni kwa sababu wakikaa nje ya shule wanapoteza masomo na shule zetu zinapata pesa kidogo kwa sababu hazina watoto wengi kwa shule.” Alisema Wangamati.

Alisema makali ya njaa miongoni mwa jamii nyingi ndio sababu kuu ya idadi kubwa ya watoto kukosa kwenda shule, akiwahakikishia wazazi kwamba wanao watapata chakula wakiwa shuleni kutokana na mikakati ya serikali kupitia wizara ya elimu kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria masomo shuleni.

“Sababu ya wao kutokwenda shule ni kutokana na njaa na inasemekana kwamba wakichunga Ng’ombe wanakamua maziwa huko wakiuza na kunywa mengine sasa wanaona ni afadhali kuliko kwenda shule. Tunawaambia kwamba chakula kipo shuleni na pia kuna mikakati inaendelea kuleta chakula zaidi.” Alisema.

Wangamati aliwataka wadau ikiwemo wazazi pamoja na viongozi wa kidini kushirikiana na idara yake kuhakikisha kwamba watoto wote wanahudhuria masomo na kutowahusisha katika shughuli ambazo zitawafanya kusalia nje ya shule kwa manufaa yao ya baadaye.

“Tunawaambia wazazi wetu na wadau wengine ikiwemo viongozi wa kidini kwamba washirikiane nasi kuhakikisha kwamba watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule wanahudhuria masomo kwa manufaa yao ya baadaye.” Alisema.