SHULE ZA UMMA ZAPIKU ZA BINAFSI KATIKA MTIHANI WA KCPE KAUNTI YA TRANS NZOIA


Takwimu za matokeo ya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka huu zinaonyesha kuwa shule za umma zilizipiku shule za kibinafsi kinyume matokeo ya hapo awali, ambapo kati ya wanafunzi kumi na tano bora shule za kibinafsi ziliweza kuwaorodhesha wanafunzi tano pekee, washikadau wa shule za kibinafsi wakihusisha hali hiyo na makali ya kiuchumi yaliyowatatiza wazazi kulipa karo, wakiitaka serikali kuwapa mikopo isiyo na riba ya juu.
Wakiongozwa na Leonard Yegon mmoja wa wakurugenzi wa shule ya kibinafsi ya Choronok eneo bunge la Cherangani kaunti ya Trans-nzoia, wadau hao wamesema shule za kibinafsi hutegemea malipo ya karo kutoka kwa wazazi kuendesha shughuli za shule zao jambo ambalo lilihujumiwa na wazazi kutoweza kulipa karo kwa wanao kukutokana na ugumu wa kiuchumi hivyo huenda swala hilo limechangia matokeo yaliyosajiliwa na shule za kibinafsi mwaka huu.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Dennis Katenya ameelezea matokeo bora yaliyoandikishwa na wanafunzi katika shule hiyo, akisema mwanafunzi wa kwanza alizoa alama ya 410 huku shule hiyo ikipata alama ya wastani ya 243, wanafunzi wa kike wakifanya vyema katika masomo ya lugha na wavulana katika masomo ya hisabati na sayansi.
Naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo Tillah Cherop amepongeza serikali kwa mfumo mpya wa elimu nchini kupitia kwa mtaala wa CBC akisema utasaidia pakubwa kukuza talanta miongoni mwa wanafunzi nchini badala ya kutoa mafunzo ya natharia pekee.