SHULE YA UPILI YA KAPSAIT YANUFAIKA NA MRADI WA MAJI KUTOKA KANISA LA ST. GEORGES BAPTIST SOUTH CAROLINA USA.

Shule ya upili ya Kapsait eneo bunge la pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi ni moja ya shule ambazo zimenufaika na mradi wa maji ambao umefadhiliwa na kanisa la St.Georges Baptist lililo Orangeburg south Carolina nchini marekani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo kiongozi wa kanisa hilo Terry wilder alisema mradi huo katika shule ya upili ya Kapsait ambao una uwezo wa kuwanufaisha takriban wakazi alfu 3 ni moja tu ya miradi minne ya maji ambayo inanuiwa kutekelezwa na kanisa hilo katika shule mbali mbali za kaunti hiyo.

“Tuna furaha kwamba angalau tumekuwa wenye manufaa kwa jamii ya eneo hili la Kapsait kupitia mradi huu wa maji ambao utawafaidi takriban watu alfu tatu. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba jamii inapata maji safi. Tunatarajia kuchimba visima vinne katika kaunti hii.” Alisema Terry.

Ajenti wa kanisa hilo hapa nchini Bramwel Siku Njeri alisema mradi huo ni afueni kwa shule hiyo kwa kuwa utawapa wanafunzi wakati wa kujiandaa kwa ajili ya mitihani kwani  hawatalazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji maeneo mengine kauli ambayo imesisitizwa na Naomy Kiprotich.

“Mradi huu ni afueni kubwa sana kwa wanafunzi hapa kwa sababu watapata wakati mzuri wa kujiandaa kwa ajili ya mitihani yao kwani sasa hawatalazimika kutoka shuleni kwenda kutafuta maji kwingine.” Walisema.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Monica Katumet alipongeza wadau waliofanikisha mradi huo akisema shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kuu ya maji ambayo ilipelekea wanafunzi kugoma kwa wakati mmoja kutokana na ugumu wa kupata bidhaa hiyo muhimu.

Kwa upande wake waziri wa maji kaunti hiyo Lucky Litole alisema serikali ya kaunti itaendeleza ushirikiano na wahisani zaidi ili kuhakikisha kwamba maisha ya wakazi yanaimarika.

“Tunafanya kazi kwa ukaribu sana na wahisani wetu kwa sababu bila uhusiano mwema hatungeweza kupata usaidizi kwa kiwango hiki. Huu mradi umeweza kutatua matatizo mengi sana ambayo shule hii imekuwa ikipitia.” Alisema Litole.