SHULE YA UPILI YA CHEWOYET YAENDELEZA MATOKEO BORA KATIKA MTIHANI WA KCSE POKOT MAGHARIBI.
Shule mbali mbali za upili katika kaunti ya Pokot magharibi zimeendelea kusherehekea matokeo bora ambayo zimesajili katika mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE mwaka jana ambayo yalitangazwa jumatatu na waziri wa elimu Ezekiel Machogu.
Miongoni mwa shule ambazo zilisajili matokeo bora kwenye mtihani huo ni shule ya upili ya wavulana ya Chewoyet ambayo kulingana na matokeo hayo mwanafunzi wa kwanza alisajili alama ya A, 24 wakisajili alama A-, 56 B+, wanafunzi 90 wakisajili alama ya B, 75 B-, C+ 50, C 12 huku mmoja akipata C-.
Naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo Amos Gesike alitaja ushirikiano miongoni mwa walimu, wanafunzi pamoja na wadau wote katika shule hiyo kuwa chanzo cha matokeo hayo mema.
“Tunamshukuru Mungu kufuatia matokeo bora ambayo tumerekodi kama shule katika mtihani wa kitaifa KCSE. Matokeo haya bora yametokana na nidhamu miongoni mwa wanafunzi, bidii na ushirikiano miongoni mwa wadau wote.” Alisema Gesike.
Ni matokeo ambayo yamepongezwa na wanafunzi pamoja na wazazi wa shule hiyo ambao waliyataja kuwa matokeo ya nidhamu na kumtii mwenyezi Mungu.
“Ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu ambapo tumeweza kusajili matokeo haya bora. Kama wazazi wa shule hii tunafurahia sana matokeo haya.” Walisema.
Hadi kufikia sasa, shule ya Chewoyet inaongoza kwa kusajili alama ya jumla ya 8.7, ikifuatiwa na shule ya upili ya wasichana ya Koporoch kwa alama 7.9, Kapenguria boys imesajili 7.78, Masol 7.57, Ptoo girls 7.53, Annet 7.08, St Comboni Amakuriat 6.85, St Catherine Chepnyal 6.85, shule ya mseto ya Chorwai 6.85 na kisha Mtelo girls ikifunga kumi bora kwa alama ya jumla ya 6.78.