SHULE YA ST MARYS YATOA MWANAFUNZI BORA WA KCPE KUFIKIA SASA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI

Walimu wazazi na wanafunzi wa shule mbali mbali kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kusherehekea matokeo bora ya mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE yaliyotangazwa rasmi hiyo jana na waziri wa elimu Prof. George Magoha.

Kulingana na matokeo ambayo yamefikia shule mbali mbali kaunti hii ya Pokot magharibi, kufikia sasa shule ya msingi ya St Marys inaongoza ambapo mwanafunzi wa kwanza aliibuka na alama 410 wa pili akipata 389 huku wa tatu akipata alama 384.

Katika shule ya Kapenguria town view academy mwanafunzi wa kwanza  kwa Jina Esther Cheptoo alipata alama 409, huku akisema kuwa juhudi zake na mchango mkubwa wa walimu ulimwezesha kupata alama hizo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Makos Lomuket amesema licha ya changamoto ya janga la corona, ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi ndio ulioleta ufanisi huo.

Katika shule ya msingi ya Nasokol mwanafunzi wa kwanza ni Ruth Chelimo Kikwai ambaye alipata alama 400 huku Lipale Shalom Chepchumba kutoka shule ya msingi ya Central academy akiibuka wa kwanza kwa alama 395.