Shule ya Sangak yakabidhiwa wizara ya elimu, wakazi wakihimizwa kukumbatia elimu

Gavana Simon Kachapin akikagua madarasa kwenye shule ya Sangak, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Wakazi wa eneo la lami Nyeusi eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuwapeleka wanao shuleni hasa baada ya kujengwa shule ya Sangak, ili wapate elimu ambayo itawafaa katika maisha yao ya baadaye.
Ni wito wake gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin baada ya kuikabidhi rasmi wizara ya elimu shule hiyo ambayo ilijengwa kwa ufadhili wa mamlaka ya barabara kuu nchini KeNHA, ambaye aidha alisema kwa ushirikiano na wadau wengine watahakikisha shule hiyo inatimiza malengo yaliyokusudiwa.
“Tutashirikiana na wadau wote kuona kwamba shule hii inafanya vyema. Na tumewaambia wakazi wa eneo hili kwamba njia ya kushukuru ni kuhakikisha wamewaleta watoto katika shule hii ili wapate elimu,” alisema Kachapin.
Aidha Kachapin alisema, kando na kuhakikisha elimu kwa wakazi, shule hiyo pia ni muhimu katika kuhakikisha amani inadumishwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo la mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana.
“Hii shule pia itachangia kuona kwamba usalama unadumishwa eneo hili ikizingatiwa ipo kwenye mpaka wa kaunti yetu ya Pokot magharibi na majirani zetu wa Turkana,” alisema.
Kauli yake ilisisitizwa na mbunge wa eneo hilo la Sigor Peter Lochakapong ambaye aidha aliipongeza serikali kwa kujenga shule hiyo aliyosema itakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi.
“Shule si shule bila ya wanafunzi kwa sababu ikisalia hivi itakuwa tu mijengo na hiyo haitakuwa shule. Kwa hivyo tunashukuru serikali kwa kutujengea shule hii hapa na tunajua itawafaa sana watu wetu,” alisema Lochakapong.