SHULE YA MSINGI YA KOPOCH YANUFAIKA NA CHAKULA KUTOKA AFISI YA MKEWE RAIS.

Shule ya msingi ya Kopoch eneo bunge la kapenguria kaunti ya Pokot magharibi imepokea chakula kutoka kwa afisi ya mkewe rais Rachael Ruto chini ya mpango wa mama doing good ambao hasa unalenga kuwanufaisha wanafunzi.

Akizungumza baada ya kupokeza shule hiyo chakula hicho Samwel Kongo ambaye anahudumu katika afisi ya mkewe rais alisema kwamba mpango huo ambao hasa unalenga shule za maeneo kame nchini unalenga kuhakikisha kwamba watoto wote maeneo hayo wanahudhuria masomo.

“Mpango huu ambao unaendeshwa na afisi ya mama wa taifa unalenga hasa kaunti za maeneo kame nchini, kuhakikisha kwamba wanafunzi wote ambao labda waliacha masomo kutokana na njaa wanarejea shuleni.” Alisema Kongo.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na afisa wa mipango katika afisi hiyo Josephat wangila ambaye aidha alitoa wito kwa wazazi eneo hilo kutosalia na wanao nyumbani kwa kisingizo cha kukosa chakula, na badala yake kuwapeleka shuleni kwani sasa kuna chakula cha kutosha, akiahidi mpango huo kuendelea.

“Nawahimiza wazazi ambao labda wako nyumbani na wanao kutokana na changamoto ya kupata chakula, kuhakikisha kwamba wanawapeleka shuleni kwani sasa kuna chakula cha kutosha na afisi ya mkewe rais imeahidi kuendeleza mpango huu.” Alisema Wangila.

Wadau katika shule hiyo wakiongozwa na mwalimu mkuu Samwel Petot walipongeza msaada huo wakiutaja kuwa muhimu zaidi katika kuhakikisha wanafunzi wanasalia shuleni hasa ikizingatiwa kwamba nyingi ya familia eneo hilo zinakabiliwa na changamoto ya kupata chakula.

“Tunashukuru sana afisi yake Bi. Rachael Ruto kwa msaada huu. Utakuwa wenye umuhimu mkubwa sana kwetu kwani utasaidia kuhakikisha watoto wanakuja shuleni.” Walisema.